RESEARCH AD

RESEARCH AD

CLEARING AND FORWADING

CLEARING AND FORWADING

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

THE GUARDIAN LTD

Wednesday, September 19, 2012

BODI YA MIKOPO (HESLB) YATANGAZA ONGEZEKO LA MIKOPO KWA WANAFUNZI HUKU WANAFUNZI 4,000 WAKIKOSA MIKOPO

WANAFUNZI 3,937 waliodahiliwa kuanza masomo ya elimu ya juu mwaka 2012/13 katika vyuo mbalimbali nchini, wamekosa mikopo kutokana na ufinyu wa bajeti.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Asangye Bangu alizungumza Dar es Salaam jana kuwa wanafunzi waliokidhi vigezo vya kupata mikopo hiyo ni 33,050 lakini waliopata ni 29,113.
Alisema kati ya wanafunzi hao waliofanikiwa kupata mikopo, wasichana ni asilimia 31.9 na wavulana asilimia  68.0.

“Jumla ya wanafunzi 49,895 walituma maombi Bodi mwaka huu. Waliokidhi vigezo na kustahili kupata mikopo ni 33,050. Wapo ambao hawatapata licha ya kukidhi viwango kutokana na ufinyu wa bajeti na masomo yao kutokuwa na kipaumbele,” alisema Bangu.

Alisema wanafunzi 28,454 tayari wameshapangiwa viwango vya mikopo na wengine 659 bado kupangiwa kutokana na kushindwa kukamilisha baadhi ya vitu ambavyo vinapaswa kuambatanishwa na fomu.

Bangu alisema vipaumbele vimewekwa kwa wanafunzi  wenye uhitaji wa mikopo hiyo kutokana na uwezo sambamba na wanaochukua kozi za ualimu, uhandisi, sayansi ya kilimo, sayansi ya wanyama, sayansi ya tiba na hisabati.
“Tumezingatia zaidi uhitaji wa mwombaji na masomo yenye vipaumbele kwanza kabla ya masomo mengine. Vilevile wapo watakaokosa kutokana na ufinyu wa bajeti,” alisema Bangu na kuongeza:

Waliofanikiwa kupata mikopo kwa masomo ya ualimu ni 13,004. Fani nyingine na idadi ya wanafunzi waliopata mikopo kwenye mabano ni uhandisi (2,369), elimu - sayansi (2,146), sayansi ya kilimo (433), sayansi ya wanyama (91), elimu - hisabati (242), sayansi ya tiba (1,583) na wanafunzi 6,838 kwa kozi zisizo za kipaumbele.

Alisema takwimu za mwaka huu zinaonyesha kuwa idadi ya wanafunzi waliopata mikopo imeongezeka kwa asilimia 12 ikilinganishwa na mwaka jana ambao waliopata walikuwa 26,000... “Serikali imetenga Sh345 bilioni ikilinganishwa na mwaka jana ambapo zilikuwa Sh317 bilioni,” alisema.

Aliwataka wanafunzi 659 ambao fomu zao zina matatizo kufanya marekebisho ndani ya siku 14 kuanzia jana ili bodi iendelee na mchakato wa kuwapitishia mikopo... “Wale ambao watakuwa wana matatizo, majina yao yatakuwa kwenye tovuti ya bodi ni vyema wangekamilisha mapema ili kuondokana na usumbufu.”
 
Chanzo: www.mwananchi.co.tz

No comments: