WASOMI WADAI MABADILIKO MITIHANI YA SEKONDARI NI SIASA TU
Siku moja baada ya Serikali kutangaza kupunguza viwango vya ufaulu kwa mtihani ya kidato cha nne na sita, baadhi ya wasomi na wadau wa elimu wameponda uamuzi huo na kusema una malengo ya kisiasa.
Baadhi ya wadau hao wakizungumza na gazeti hili
jana, walisema Tanzania imeweka rekodi kwa nchi za Afrika kwa kuwa na
kiwango kidogo sana cha ufaulu cha alama F kuanzia 0 mpaka 19.
Walisema, Serikali imechukua uamuzi huo kisiasa
ili kuhakikisha kuwa, wanatimiza lengo la Mpango wa Maendeleo Makubwa
Sasa (BRN), ambalo ni kuhakikisha matokeo ya ufaulu kwa Mtihani wa
Kidato cha Nne mwaka huu yanafikia asilimia 60 kutoka 33 ya mwaka jana.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Profesa Herme Mosha alisema kuwa kilichofanywa na Serikali ni
kupanua wigo wa watu kufaulu.