WARIOBA ATAKA ELIMU CHUO KIKUU IBORESHWE
Rais wa Umoja wa waliokuwa wanafunzi wa Chuo Kkuu cha Dar es Salaam, Jaji Mstaafu Joseph Warioba amewataka wahitimu wa chuo hicho kuungana kukisaidia kuboresha miundombinu na ubora wa elimu.
Jaji Warioba, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba alisema hayo juzi wakati umoja huo walipokutana
kujadiliana jinsi ya kuboresha chuo hicho kwa kutoa michango yao pasipo
kusubiri jukumu hilo kufanywa na Serikali.
Warioba alisema hali ya chuo ni ngumu kutokana na
kuchakaa kwa miundombinu mbalimbali, uhaba wa walimu na vitendea kazi,
jambo ambalo aliwataka kuunganisha nguvu kusaidia mabadiliko.
“Tukishirikiana tutahakikisha tunawasaidia
wanafunzi wetu, pia michango yetu itaboresha elimu na kuleta
mabadiliko,” alisema Jaji Warioba aliyesoma chuoni hapo miaka 50
iliyopita. Alisema tangu umoja huo ulipoanzishwa, zaidi ya Sh 2bilioni
zimekusanywa na zote zimeelekezwa katika uboreshaji wa elimu chuoni
hapo.
Akifafanua, Warioba alisema Rais wa Uganda, Yoweri
Museveni aliandaa chakula cha jioni nchini humo, ambapo zaidi ya Sh350
milioni zilipatikana na kuahidi kuchangia zaidi sambamba na Rais Jakaya
Kikwete.
Kwa upande wake, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo hicho,
Profesa Florens Luoga alisema lengo la chuo ni kuwashirikisha wahitimu
kurudisha fadhila kwa kuchangia katika kuboresha seka ya elimu chuoni
hapo.
Profesa Luoga alisema kutokana na chuo hicho kuwa
kikongwe na kuzaa vyuo vingine nchini, jakumu kubwa kwao ni kuhakikisha
wanavisaidia vyuo hivyo kufikia malengo yao.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment