SERIKALI YAWEWESEKA NA ''ZIRO'' YAKE
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge Mh. William Lukuvi |
KATIKA kile kinachoonekana kuwa ni kuweweseka kwa serikali
katika sakata la kufuta daraja sifuri katika mitihani ya kidato cha nne
na sita, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na
Bunge), William Lukuvi, jana alilazimika kumkana Katibu Mkuu wa Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome.
Lukuvi alisema taarifa aliyoitoa Mchome wiki iliyopita kuwa serikali
imefuta daraja sifuri kwa kidato cha nne na sita haikuwa ya serikali,
bali ile iliyotolewa juzi na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Philip Mulugo, kuwa haijafutwa ndiyo sahihi.
Lukuvi alitoa kauli hiyo mara baada ya Mbunge wa Kawe, Halima Mdee
(CHADEMA), kuomba mwongozo wa Spika akitaka kujua hatua
watakazochukuliwa mawaziri wa wizara hiyo kwa kulidanganya Bunge na
umma.
Mdee alitumia mwongozo wa kanuni ya 68 (7) sambamba na kanuni ya 63
(1) inayosomeka kuwa; ‘Bila kuathiri masharti ya ibara ya 100 ya katiba
inayolinda na kuhifadhi uhuru na mawazo katika Bunge ni marufuku
kabisa kuongea uongo bungeni.’
Alibainisha kuwa kanuni hiyo inasema mbunge yeyote anapokuwa amesema
uongo bungeni, ana wajibu wa kuhakikisha kwamba anatoa kauli au maelezo
kuhusu jambo au suala ambalo yeye mwenyewe anaamini kuwa ni la kweli,
na si la kubuni au kubahatisha.
Mdee alisema juzi Naibu Waziri Mulugo, alilihadaa Bunge kwa kukanusha
kuwa wizara imefuta daraja sifuri huku akivitupia lawama vyombo vya
habari na mitandao ya kijamii kwa kuandika na kujadili taarifa hiyo, na
kudai kuwa ni uzushi ambao hauna ukweli.
Mbunge huyo alisema Mulugo alikuwa akipishana na katibu mkuu wa
wizara yake ambaye alitoa maelezo ya mabadiliko ya upangaji wa madaraja
uliokuwa ukionyesha serikali kufuta daraja sifuri.
Alisema nyaraka alizonazo ambazo Profesa Mchome alizitolea taarifa ya
mabadiliko hayo, zinaweka wazi kuwa serikali imefuta daraja sifuri na
kuweka daraja linalojulikana kama daraja la tano, ambalo litakuwa
daraja la mwisho katika ufaulu.
“Naomba mwongozo wako, Naibu Spika…utuambie, kauli kama hizi za
uongo, za kubahatisha zinazotolewa na waziri zinachukuliwa hatua gani,
na kwakuwa kauli za mawaziri hazijadiliwi na kwa kuzingatia waziri
anaonekana hata jambo lenyewe halijui, hudhani kwamba ni muhimu
tukalijadili jambo hili?” alihoji.
Katika maelezo yake, Lukuvi alisema kauli ya waziri ndiyo ya serikali
na si kauli ya katibu mkuu, hivyo ni vema wananchi wakachukua kile
kilichosemwa na waziri.
“Alichokisema Mdee ndicho kilichosemwa jana na naibu waziri, lakini
akisimama hapa naibu waziri anasimama kama serikali, na kwa mfumo wa
utawala serikalini, waziri ndiye mwenye mamlaka, hivyo kwa mantiki hiyo
kauli ya serikali inakuwa ile ya waziri na si ya katibu mkuu,”
alisema.
Hata hivyo, Lukuvi alisema kuwa serikali inajiandaa kutekeleza agizo
lililotolewa juzi na Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuitaka ipeleke
bungeni maelezo juu ya jambo hilo ili kuondoa mkanganyiko uliojitokeza.
Mara baada ya Waziri Lukuvi kutoa maelezo hayo, Naibu Spika, Job
Ndugai, aliitaka serikali kuharakisha mchakato wa kupeleka bungeni
taarifa ya serikali kuhusu ufafanuzi wa upangwaji wa madaraja.
“Na mimi nasisitiza katika hili, kauli iletwe na serikali haraka,
kwakuwa vijana wanafanya mtihani hivi sasa, na hawajui hata kile
wanachofanya ni kitu gani katika upande wa madaraja, kwa hiyo hili ni
jambo la haraka, mliletee ufafanuzi mapema,” alisema Ndugai.
No comments:
Post a Comment