RESEARCH AD

RESEARCH AD

CLEARING AND FORWADING

CLEARING AND FORWADING

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

THE GUARDIAN LTD

Tuesday, November 5, 2013

Maaskofu wapinga alama mpya za mitihani

Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (Tec), ‘limeuponda’ uamuzi wa serikali wa kushusha viwango vya ufaulu kwa mitihani ya kidato cha nne na sita, likisisitiza kuwa hatua hiyo ni upungufu na ishara ya kuporomoka kwa siasa na ni kipimo kitakachoitumbukiza elimu shimoni.
Kauli hiyo ya Tec, imekuja wakati serikali imetangaza rasmi kuanza kutumika kwa mfumo mpya wa usahihishaji wa mitihani na upangaji wa viwango vya madaraja ya ufaulu, uamuzi ambao hata hivyo, umelifuta daraja sifuri, kuanzia mwakani.

Rais wa baraza hilo, Askofu Tarcius Ngalalekumtwa, akizungumza katika mahafali ya sita ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu, Mwenge (Mwuce), kilichopo Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, alisema kitendo hicho kinaishangaza dunia kutokana na wenye dhamana kubadili maneno katika kushughulikia elimu na kwamba hali siyo nzuri katika sekta hiyo kwa sababu 'hatutaki kutafuta ni wapi tulipojikwaa na kutufikisha hapo tulipo.'

Mabadiliko hayo na utaratibu wa kuimarisha mfumo huo wa ufaulu, utaanza kutumika katika kupanga matokeo ya kidato cha nne na sita kwa
mwaka 2013/2014, wakati umma ukiwa bado unahoji kilicho nyuma ya pazia juu ya matokeo ya aibu ya mwaka jana ya kidato cha nne baada ya asilimia 60 ya watahiniwa wote kupata daraja sifuri.


“Kufuta zero (sifuri), ni sawa na kuongeza zero nyingine kwa kuwa utazalisha wengi wasio na sifa hata kama utabadili maneno na kuliita daraja fulani; tunalitumbukiza taifa letu katika balaa. Hali si nzuri na hatujui hali hiyo ilianza lini ingawa kuna mahali tulipita na kujikwaa…huu ni upungufu na kuporomoka kwa siasa,” alisema Rais huyo.

Alienda mbali zaidi, akiitaka serikali kutazama upya suala la mikopo kwa wanafunzi wanaodaihiliwa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu nchini,
kutokana na vijana wengi kukosa mikopo hiyo kwa kisingizio cha kushindwa kukidhi vigezo vya bodi ya mikopo ambayo imekuwa ikikabiliwa na mapungufu kadhaa.

Awali, Mwenyekiti wa bodi ya chuo hicho ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, Askofu Isack Amani, akitoa nasaha zake katika mahafali hayo, alisema taifa linapaswa kutafakari upya uamuzi huo kwa kuwa watu wanaweza kufuta mawazo ya alama sifuri usoni lakini siyo kichwani.

“Wakati Watanzania wanatafakari uamuzi huu wa serikali, naomba nikuhakikishe, baba askofu Ngalalekumtwa (Rais wa Tec), kwamba maagizo ya baraza lako kuhusu chuo hiki (Mwuce)  kuwa chuo kikuu kamili, menejimenti iko katika mchakato huo na tutakuita ukizindue mara baada ya kupata hati ya ithibati toka Tume ya Vyuo Vikuu nchini yaani TCU,” alisema Askofu Amani.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut), cha Jijini Mwanza, Padri Pius Mgeni, akizungumzia mustakabali wa elimu nchini kwa sasa, alisema kwamba hali ni mbaya katika baadhi ya vyuo vya elimu ya juu kutokana na idara nyingi ikiwamo inayoshughulikia lugha ya Kiswahili kuongozwa na wageni kutoka nje ya nchi kutokana na wazawa kukosa sifa za kuongoza baadhi ya idara.

“Ukimsikia mtu anakuita wewe ni Mswahili usifikiri anakusifia unajua Kiswahili, hapana; huyo anamaanisha wewe hujui na ni mtu wa porojoporojo.

Hali ni mbaya vyuoni na hata pale kwangu idara ya Kiswahili inaongozwa na Wakenya wakati sisi tunapiga blaa blaa. Tunalo tatizo kwa sababu wasomi wanakimbizana na fedha badala ya kutoa mchango wao kwa taifa,” alisema Padre Mgeni.

Hata hivyo, baadhi ya wahitimu wa chuo hicho waliozungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti, walisema serikali imechukua uamuzi huo kisiasa ili kuhakikisha inatimiza lengo lao la mpango wa matokeo makubwa sasa, ambalo ni kuhakikisha matokeo ya ufaulu kwa mtihani wa kidato cha nne mwaka huu unafikia asilimia 60 kutoka 33 ya mwaka jana.

Jumla ya wahitimu 447 walitunukiwa vyeti vya ngazi mbalimbali kwenye mahafali hayo.

Awali, Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) lilikuwa likitumia alama A, B, C, D na F huku alama A ikianza na maksi wa asilimia 81-100, B=61-80, C=41-60, D=21-40 na F=0-20. Aidha kulikuwapo na madaraja ya I, II, III, IV na 0.

Kwa mujibu ya mabadiliko hayo yaliyotangazwa wiki iliyopita na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome, alama zitashuka ambapo alama A itakuwa ni (75-100),B+ (60-74), B (50-59),C (40-49), D (30-39), E (20-29) na F (0-19).


Chanzo: NIPASHE

No comments: