BODI YA MIKOPO (HESLB) YATANGAZA ONGEZEKO LA MIKOPO KWA WANAFUNZI HUKU WANAFUNZI 4,000 WAKIKOSA MIKOPO
WANAFUNZI 3,937 waliodahiliwa kuanza masomo ya elimu
ya juu mwaka 2012/13 katika vyuo mbalimbali nchini, wamekosa mikopo
kutokana na ufinyu wa bajeti.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi
ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Asangye Bangu
alizungumza Dar es Salaam jana kuwa wanafunzi waliokidhi vigezo vya
kupata mikopo hiyo ni 33,050 lakini waliopata ni 29,113.
Alisema kati ya wanafunzi hao waliofanikiwa kupata mikopo, wasichana ni asilimia 31.9 na wavulana asilimia 68.0.
“Jumla
ya wanafunzi 49,895 walituma maombi Bodi mwaka huu. Waliokidhi vigezo
na kustahili kupata mikopo ni 33,050. Wapo ambao hawatapata licha ya
kukidhi viwango kutokana na ufinyu wa bajeti na masomo yao kutokuwa na
kipaumbele,” alisema Bangu.
Alisema wanafunzi 28,454 tayari
wameshapangiwa viwango vya mikopo na wengine 659 bado kupangiwa kutokana
na kushindwa kukamilisha baadhi ya vitu ambavyo vinapaswa
kuambatanishwa na fomu.
Bangu alisema vipaumbele vimewekwa kwa
wanafunzi wenye uhitaji wa mikopo hiyo kutokana na uwezo sambamba na
wanaochukua kozi za ualimu, uhandisi, sayansi ya kilimo, sayansi ya
wanyama, sayansi ya tiba na hisabati.
“Tumezingatia zaidi uhitaji wa
mwombaji na masomo yenye vipaumbele kwanza kabla ya masomo mengine.
Vilevile wapo watakaokosa kutokana na ufinyu wa bajeti,” alisema Bangu
na kuongeza:
Waliofanikiwa kupata mikopo kwa masomo ya ualimu ni
13,004. Fani nyingine na idadi ya wanafunzi waliopata mikopo kwenye
mabano ni uhandisi (2,369), elimu - sayansi (2,146), sayansi ya kilimo
(433), sayansi ya wanyama (91), elimu - hisabati (242), sayansi ya tiba
(1,583) na wanafunzi 6,838 kwa kozi zisizo za kipaumbele.
Alisema
takwimu za mwaka huu zinaonyesha kuwa idadi ya wanafunzi waliopata
mikopo imeongezeka kwa asilimia 12 ikilinganishwa na mwaka jana ambao
waliopata walikuwa 26,000... “Serikali imetenga Sh345 bilioni
ikilinganishwa na mwaka jana ambapo zilikuwa Sh317 bilioni,” alisema.
Aliwataka
wanafunzi 659 ambao fomu zao zina matatizo kufanya marekebisho ndani ya
siku 14 kuanzia jana ili bodi iendelee na mchakato wa kuwapitishia
mikopo... “Wale ambao watakuwa wana matatizo, majina yao yatakuwa kwenye
tovuti ya bodi ni vyema wangekamilisha mapema ili kuondokana na
usumbufu.”
Chanzo: www.mwananchi.co.tz